Sunday, October 9, 2011

Poulsen ataja First XI

Taifa Stars
Kocha Jan Poulsen ametaja kikosi cha wachezaji 11 ambao wataanza kwenye mechi ya leo dhidi ya Morocco. Mechi hiyo inaanza saa 1.30 usiku kwa saa za hapa ambapo nyumbani Tanzania ni saa 4.30 usiku na itachezwa Grand Stadium hapa Marrakech. Poulsen atatumia mfumo wa 4-4-1-1 huku akimweka Mbwana Samata kuwa mshambuliaji wa mwisho na nyuma yake akicheza Abdi Kassim.
Katika kikosi cha kwanza amewaanzisha wachezaji wote wa kulipwa wanaocheza nje ya Tanzania ambao anao hapa. Amewataka wachezaji kuwa focussed na mchezo, kujituma na kila mmoja kutekeleza wajibu wake uwanjani ili ushindi uweze kupatikana. Baada ya kutoa game plan yake, Poulsen aliwaonesha wachezaji CD ya mechi ya kwanza nyumbani dhidi ya Morocco ambapo tulifungwa bao 1-0.
Kupitia CD hiyo aliwaeleza wachezaji upungufu uliojitokeza na pia wachezaji hatari wa Morocco wanaotakiwa kuangaliwa kutokana na uzuri wao wanapokuwa uwanjani. Amewakumbusha mabeki kuwa mshambuliaji Chamakh Marouane (Arsenal, Uingereza) kuwa ni mzuri kwa mipira ya vichwa, hivyo kutomuacha kuruka peke yake katika mipira hiyo.
Stars: Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Idrisa Rajab, Juma Nyoso, Aggrey Morris, Shabani Nditi, Mohamed Rajab, Henry Joseph (Captain), Mbwana Samata, Abdi Kassim na Dan Mrwanda.

Subs: Shabani Dihile, Nassoro Cholo, John Bocco, Ramadhan Chombo, Mrisho Ngasa, Nadir Haroub, Jabir Aziz

Iniesta nje Mwezi Mmoja


 
 
Klabu ya Barcelona imetangaza kwenye mtandao wake kwamba, Andres Iniesta atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa mwezi mmoja.

Kiungo huyo aliumia dakika 5 kabla ya mapumziko, kwenye mechi ambayo timu yake ilitoka sare ya 2-2 na AC Milan, katika michuano ya Kombe la mabingwa Barani Ulaya siku ya Jumanne.

Iniesta atakosa mechi dhidi ya Osasuna, Valencia, Atletico Madrid, BATE Borisov na Sporting Gijon.

Mchezaji huyo anategemea kurudi tena uwanjani kwenye mechi ya michuano ya Euro 2012, ambapo timu ya Hispania itakapocheza na Czech Republic na Scotland, mnamo tarehe 7 na 11 Oktoba.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, ameweza kucheza jumla ya mechi 6 kwa klabu msimu huu, huku akikamilisha wastani wa dakika 469 uwanjani.

Bradley aajiriwa Misri

 
 
Inaarifiwa kwamba, Kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Marekani Bob Bradley, ameajiliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Misri.

Msemaji wa EFA Azmy Megahed amesema, Bradley anategemea kuwasili Cairo wikiendi hii kukamilisha mpango huo.

"Kila kitu kipo sawa. Bradley atawasili hapa siku ya Jumapili kukamilisha mkataba," Megahed alisema.

Bradley atakuwa amechukua nafasi ya kocha wa kipindi kirefu wa timu hiyo Hassan Shehata, ambaye kibarua chake kilisitishwa mnamo mwezi June, kufuatia kufanya vibaya kwa timu hiyo kwenye kampeni zake za kushiki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mwaka 2012.

Timu hiyo mpaka sasa imetolewa kwenye mbio hizo.

Bradley aliiwezesha Marekani kufika kwenye mzunguko wa 16 wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2010, iliyofanyika nchini Afrika ya Kusini.

Na alipigwa chini mnamo mwezi July baada ya Marekani kufungwa 4-2 na Mexico kwenye fainali ya Gold Cup, huku nafasi yake ikichukuliwa na kocha wa zamani wa Ujerumani Jurgen Klinsmann.

Bradley atakuwa na mtihani mzito kuhakikisha nchi ya Misri inapata nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia, kwa mara ya mwisho Taifa hilo kushiriki Kombe hilo ilikuwa ni mwaka 1990.
.
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Polisi Dodoma iliyochezwa Septemba 14 mwaka huu Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam imeingiza sh. 16,839,000.

Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 2,257 ambapo kiingilio kilikuwa sh, 7,000 kwa mzunguko na sh. 20,000 kwa VIP. Waliokata tiketi za sh. 20,000 walikuwa 80.

Baada ya kuondoa gharama za mchezo na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 2,568,661.02 kila timu ilipata sh. 3,546,671.90. Mgawo mwingine ulikwenda kwa uwanja (sh. 1,162,893.90), TFF (sh. 1,162,893.90), Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu- FDF (sh. 581,446.95), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam- DRFA (sh. 465,157.56) na Baraza la Michezo la Taifa- BMT (sh. 116,289.39).
Wayne Rooney
 
Meneja wa klabu ya Manchester United Sir Alex Ferguson, amemfananisha mshambuliaji wa timu yake Wayne Rooney na mchezaji mkongwe wa Brazil Pele.

Fergie ameyasema hayo, kuelelekea kwenye mechi ya Kombe la Klabu Bingwa ya Ulaya dhidi ya Benfica, mechi inayotarajiwa kuchezwa usiku huu, huku mchezaji huyo akionekana kuwa kwenye kiwango kizuri kiuchezaji.

Upatikanaji wa Tiketi mechi za Simba na Yanga Uwanja wa Chamazi

Tiketi kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom zinazohusisha timu za Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam hazitauzwa uwanjani. Lengo ni kuwaondolea usumbufu mashabiki ambao wanakwenda kwenye mechi hizo na kukuta tiketi zimekwisha, hivyo kuweza kuwa chanzo cha vurugu.

Ili kujiridhisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lilifanya uhakiki na kubaini Uwanja wa Azam una uwezo wa kuchukua watazamaji 5,000 tu na si 7,000 kama ilivyoelezwa awali. Hata hivyo lengo la mmiliki wa uwanja huo ni kuongeza viti hadi kufikia 7,500.

Kwa mantiki hiyo tiketi zitakazouzwa kwa mechi za Yanga na Simba kwenye uwanja huo ni 5,000 tu. Vituo vya kuuzia tiketi hizo siku moja kabla ya mchezo na siku yenyewe ya mchezo ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kituo cha Mafuta cha OilCom kilichoko Ubungo na Mbagala Rangitatu.

Viingilio kwa mechi za timu hizo zitakazochezwa Uwanja wa Azam ni sh. 20,000 kwa jukwaa kuu lenye uwezo wa kuchukua watazamaji 400 wakati majukwaa ya kawaida itakuwa sh. 7,000. Ili kuhakikisha idadi ya mashabiki haizidi uwezo wa uwanja hakutakuwa na tiketi za bure (complimentary).

Hivyo kutokana na kuwepo vituo vya kuuzia tiketi katika maeneo yaliyotajwa, mashabiki ambao watakosa tiketi hawana sababu ya kwenda uwanjani. Simba na Yanga zitaanza kuutumia uwanja huo kesho (Septemba 14 mwaka huu) kwa Simba kuwa mwenyeji wa Polisi Dodoma wakati siku inayofuata Yanga itakuwa mgeni wa African Lyon.

Sendeu kwa Pilato Tibaigana

Luis Sendeu
 
Sekretarieti ya TFF itawasilisha mashtaka dhidi ya Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi inayoongozwa na Kamishna wa Polisi mstaafu Alfred Tibaigana kutokana na matamshi yake dhidi ya mwamuzi Alex Mahagi.

Mara baada ya mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyochezwa Septemba 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1, Sendeu aliita mkutano na waandishi wa habari na kumshutumu Mahagi kuwa alisababisha timu yake ikose ushindi kwa kuwabeba wapinzani wao.

Aliongeza kuwa anamfahamu Mahagi kuwa ni mwanachama wa Simba, kadi nyekundu aliyompa kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima si halali na alifanya hivyo kwa lengo la kuisadia Simba ili iendelee kukaa kileleni mwa ligi.

Kauli ya Sendeu ililenga kumjengea chuki Mahagi mbele ya mashabiki wa Yanga kama ilivyo kwa viongozi na watendaji wa TFF. Ni wazi Sendeu akiwa ofisa wa Yanga anajua taratibu za kufanya pale klabu yake isiporidhishwa na uamuzi wa mwamuzi au suala lingine lolote.

Matamshi ya Sendeu yanalenga kuchochea chuki na vurugu katika mpira wa miguu ambapo ni kinyume na Ibara ya 53(1) na (2) ya Kanuni za Nidhamu za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).