Friday, September 2, 2011

Taifa Stars Lazma Kieleweke LEO


Kikosi Cha Stars

KIKOSI cha Taifa Stars kinaingia leo uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kupambana na Algeria katika mechi ya kuwania kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika.

Hii ni mechi ya marudiano kwa timu hizi kwa sababu katika mechi ya kwanza iliyofanyika kwenye uwanja wa Mustafa Tchaker uliopo mjini Blida kilomita 45 kutoka katika mji wa Algiers, Taifa Stars ilitoka sare1-1.

Mpaka sasa kikosi cha Taifa Stars kimepoteza mechi mbili katika mechi nne kilichocheza katika kutafuta nafasi ya kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika 2012 zitakazofanyika kwenye nchi za Gabon na Guinea ya Ikweta.

Mechi ya mwisho Taifa Stars ilishindwa kutamba mbele ya timu ya Jamhuri ya Afrika ya Kati baada ya kuchapwa mabao 2-1 kwenye uwanja wa Barthelemy Boganda mjini Bangui.

Kutokana na kupoteza mechi hiyo Taifa Stars hivi hivi sasa ipo katika nafasi ngumu ya kufuzu kushiriki fainali hizo za Afrika, ambapo imebakisha mechi mbili ambazo inatakiwa kushinda mechi zote ili ifikishe pointi 10 kuweza kufuzu.

Taifa Stars imebakisha mechi dhidi ya Algeria ambayo inachezwa leo jijini Dar es Salaam, pia imebakisha mechi dhidi ya Morocco ambayo itachezwa huko mjini Rabat kwenye uwanja wa Prince Moulay Abdellah kati ya tarehe 7,8,9/10/2011.

Mpaka sasa Taifa Stars imeshinda mechi moja ambayo iliifunga Jamhuri ya Afrika ya Kati mabao 2-1 katika pambano lililopigwa jijini Dar es Salaam, ilitoka sare ya bao 1-1 na Algeria, vile vile Stars ilifungwa bao 1-0 na Morocco kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kwa mechi ilizocheza Taifa Stars hivi sasa inashika nafasi ya tatu katika kundi D ikiwa na pointi nne sawa na Algeria inayoshika nafasi ya nne ikiwa na pointi nne, timu inayoshika nafasi ya kwanza katika kundi hilo ni Morocco yenye pointi saba ikifuatiwa na Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo ina pointi saba pia.

Morocco yenyewe hivi sasa imebakisha mechi dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati mechi itakayochezwa mjini Bangui pia imebakisha mechi dhidi ya Tanzania itakayochezwa mjini Rabat, wakati Jamhuri ya Afrika ya Kati imebakisha mechi dhidi ya Morocco mjini Bangui na mechi dhidi ya Algeria huko nchini Algeria.

Algeria pia imebakisha mechi ya leo dhidi ya Tanzania mjini Dar es Salaam na mechi dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati huko nchini Algeria.

Kama Morocco ikishinda mechi zote itafikisha pointi 13 na Jamhuri ya Afrika ya Kati ikishinda mechi zote itafikisha pointi 13 , hivyo Taifa Stars ina kazi kubwa ya kufanya, vile vile inatakiwa kuomba Morocco na Jamhuri ya Afrika ya Kati zifanye vibaya katika mechi zilizobakia.

Ni wazi wachezaji wetu waliochaguliwa na kocha Poulsen kuunda kikosi cha timu ya taifa hivi sasa wana kazi kubwa ya kulivusha taifa la Tanzania katika kipindi hiki kigumu ili tuweze kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika 2012.

Wachezaji wa Stars leo wanatakiwa kuingia uwanjani wakiwa na lengo moja tu la kupata ushindi siyo kutoka sare wala kufungwa.

Tunafahamu mchezaji wa timu ya taifa kazi yake ni kupigania kitu ambacho huwa na thamani na kumbukumbu kubwa kwa vizazi vingi vitakavyofuatia.

Kitu wanacholeta wachezaji wa timu ya taifa ni ushindi, siku zote wachezaji wa timu ya taifa wanaposhinda huwa wanaliletea taifa lao furaha na kujisikia fahari kuishi katika taifa hilo, hivyo tunatarajia wachezaji waliochaguliwa na kocha Jan Poulsen wataweza kutuletea furaha wananchi wa Tanzania katika mechi ya leo.

Tunaamini wachezaji wa Stars watatumia akili ya mchezo kwa ahali ya juu, nguvu na stamina waliyonayo ili kupata ushindi leo.

No comments:

Post a Comment