Sunday, September 4, 2011

TFF yachakachua Ratiba Ligi Kuu

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana lilitangaza tena kuipangua ratiba ya mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambayo inaendelea nchini katika viwanja mbalimbali.

Akizungumza jana, Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema kuwa mechi namba 19 kati ya Simba na Villa Squad (zote za Dar es Salaam), iliyopangwa kufanyika Septemba 8, sasa itachezwa Septemba 7 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Wambura alisema vilevile kuwa mechi kati ya Azam na Simba, sasa itachezwa Septemba 10 kwenye Uwanja wa Mkwakwani na hilo limetokana na nia ya kuipa unafuu Azam ambayo itakuwa ikitokea Arusha kucheza dhidi ya JKT Oljoro na kupata fursa ya kumaliza mechi zao kwenye kanda hiyo.

Wambura pia alisema kuwa Kamati ya Mashindano ya TFF imeisogeza mbele kwa siku moja mechi kati ya Coastal Union ya Tanga dhidi ya Moro United ya Dar es Salaam ambapo sasa itachezwa Septemba 8.

Imebainika kuwa ratiba ya awali iliyotolewa na kamati hiyo itakayomalizika Aprili Mosi mwakani itaendelea kupanguliwa kila mara kwani bado haijatoa nafasi kwa timu za Yanga na Simba ambazo mapema mwakani zitashiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

No comments:

Post a Comment