Kiungo mtukutu, ambaye katika siku za karibuni amekuwa kwenye mgogoro wa kinidhamu na uongozi wa klabu ya Newcastle, Joey Barton ameachana rasmi na klabu hiyo na kutua Queens Park Rangers.
Barton mwenye miaka 28, ambaye alitua Newcastle akitokea Manchester City mwaka 2007, alikuwa katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake na mapema baada ya kufunguliwa kwa dirisha la usajili msimu huu, aliwekwa sokoni baada ya kutumia mtandao wa kijamii wa Twitter kuwazodoa viongozi wake.
Wakati mchezaji mwenyewe akizungumzia uhamisho huo kama jambo muhimu lililohitajika ili kuhakikisha kuwa sakata lake na Newcastle linafikia ukingoni, taarifa fupi ya klabu ya QPR aliyojiunga nayo imeelezea usajili huo kuwa ni kwa ajili ya “kumuwezesha Barton, kuuonyesha ulimwengu wa soka kuwa yeye ni mchezaji mkubwa na atawaonyesha kile anachoweza kukifanya kwa ufasaha akiwa klabuni hapa”
Dau kamili la kiungo huyo mahiri lakini ambaye utukutu wake umekuwa ukimfanya aonekane mchezaji asiye na maana ndani na nje ya uwanja, halikutajwa lakini ni wazi kuwa QPR kama wataamua kuachana na matatizo yake ya nje ya uwanja na kutaka kunufaika na kile anachoweza kukifanya awapo uwanjani, watakuwa wamepata mmoja wa wachezaji muhimu watakaowapa nafasi ya kufanya vyema msimu huu.
No comments:
Post a Comment