Monday, August 29, 2011

TFF yazidi kuiwekea ngumu Yanga

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema linapinga makubaliano yoyote baina ya Yanga na wadhamini wa Ligi Kuu, Kampuni ya simu ya Vodacom yenye lengo la kubadilisha rangi ya nembo kwenye jezi za timu hiyo na kusema watazingatia kanuni zinazoendesha ligi hiyo kuamua suala hilo.

Kauli hiyo ya TFF inafuatia kuwapo kwa taarifa kwamba, Uongozi wa Kampuni ya Vodacom na ule wa Yanga kwa pamoja umekubaliana kubadilisha rangi ya nembo iliyopo kwenye jezi za timu hiyo kutoka nyekundu na kuwa nyeusi ili kumaliza mgogoro ulioibuka baina ya pande hizo mbili kwa upande mmoja na shirikisho hilo kwa upande mwingine.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema hatua ya shirikisho hilo kuikubalia Yanga kubadilisha rangi ya nembo kwenye jezi za timu yao ni sawa na ukiukwaji wa kanuni za Ligi Kuu ambazo zinataka timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu kuzifuata.

"Hatuwezi kukubali kuyumbishwa na timu moja, ikiwa tutaacha hali hii iendelee ni dhairi tunaweza kuwakimbiza wadhamini ambao wana nia njema ya kuendeleza soka hapa nchini.

"Sisi kama TFF tutakachoangalia hapa ni kanuni zinasemaje, kwa sababu ikiwa tutalichukulia hili suala juu juu na kuiruhusu Yanga kufanya inavyotaka inaweza kutuletea matatizo zaidi kwa sababu klabu nyingine zinaweza kujitokeza na kusema hazitaki hiki.

"Sio kweli kwamba viongozi wa klabu hizi hawajui mambo haya,wanafahamu vizuri masharti ya mdhamini isipokuwa wanafanya hivi kwa lengo la kutuyumbisha,"alisema Wambura bila kufafanua ni kanuni ipi watakayoitumia.

Hata hivyo Wambura alisema kuwa pande hizo tatu, yaani TFF,Vodacom na Yanga zitakuwa na kikao cha pamoja leo kwenye ofisi za shirikisho hilo ili kuzungumzia suala hilo.

No comments:

Post a Comment