Friday, August 26, 2011

Vodacom Miss Tanzania wazuru kaburi la Sokoine

WAREMBO 30 wanaowania taji la Vodacom Miss Tanzania, wametakiwa kuwa mabalozi na kioo kwa jamii inaowazunguka ili kuipa sifa fani hiyo, ambayo watu wengi wanaona imejaa uhuni wakati si kweli.
Ushauri huo umetolewa na diwani wa Kata ya Monduli Juu iliyopo wilayani Monduli mkoani Arusha, Bariki Sumuni wakati warembo hao walipozuru kaburi la Waziri Mkuu wa zamani hayati Edward Sokoine.
Sumuni alisema watu wengi na hasa jamii ya kimasai ilikuwa na mtazamo tofauti na mashindano ya urembo, kwani baadhi ya warembo wanapotwaa taji la MissTanzania wanafanya vitu ambavyo ni kinyume na maadili na kufanya wazazi kuendelea kuchukia fani.
Alisema kwa sasa jamii ya kifugaji ya Kimasai imeanza kuelimika ikiwa ni pamoja na kuwaruhusu watoto wao wa kike kwenda shule na hata kushiriki urembo tofauti na zamani, hivyo basi huenda miaka ijayo Miss Tanzania anaweza kuwa jamii ya kimasai na kuwakilisha
vema nchi.
‘’Sisi Wamasai watoto wa wetu wa kike zamani tulikuwa hatutaki hata waende shule, lakini kwa sasa wazazi tuko mstari wa mbele kuhakikisha watoto wetu wanaenda shule na hata kushiriki urembo,’’ alisema.
Diwani huyo aliwasifu warembo hao kwa uamuzi wao wa kulitembelea kaburi la Sokoine, kwani ni uamuzi mzuri na wanapaswa kuuenzi kwa kuiga mifano ya marehemu huyo ikiwa ni pamoja na kuiga yaliyokuwa yakifanywa enzi za uhai wake.
Alisema hayati Sokoine alikuwa muadilifu, mcha Mungu na alikuwa mstari wa mbele kulinda maadili ya mtoto wa kike kwa kujiheshimu, hivyo basi warembo hao wanapaswa kuiga mfano huo, ikiwa ni njia mojawapo ya kumuenzi kutembelea kaburi hilo.
Warembo hao pia walitembelea kampuni ya Tan Media inayomiliki kituo cha redio 5 na TV ya ABC kuijionea wenyewe namna ya uandaaji na utangazaji unaofanywa na watangazaji wa kampuni hiyo.

No comments:

Post a Comment